Saturday, January 14, 2012

Afrika itabadilika kama siasa zitamilikiwa na wapiga kura!!

"Mnaweza kuiita vyovyote, waswahili husema, 'mnyonge mnyongeni....' hili ni Vuguvugu la Mnyonge." Ilianzia Tunisia, Misri na sasa swali limebaki kuwa je itaishia Libya au kuna panapofuka moshi?

Ni swali rahisi sana, na bila shaka jibu liko wazi kwa zaidi ya asilimia 80. Binafsi nasema Moshi bado wafuka tena kwa kasi ya ajabu, hakuna aliye salama na atakae salimika kama hali itaendelea kubaki hivi ilivyo.

Ni takribia miongo sita toka nchi ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika kupata Uhuru. Hadi sasa hakuna hata nchi mmoja kutoka ukanda huo inaweza kusimama kifua mbele na kukiri kuwa imepiga hatua kimaendeleo. Umaskini uliokithiri, Rushwa, magonjwa na vita ndio sura inayotawala ramani ya bara la Afrika.

Wanasiasa wameshindwa kuja na mbinu mpya ya kukabiliana na changamoto hizi. Afrika inatajwa kuongoza kwa utitiri wa vyama vya siasa duniani. Hii peke yake inatosha kutambulisha tabia mbaya ya viongozi wetu - UCHU wa Madaraka. Siasa sasa ni mtaji wa kujitajirisha na kila anaewaza kugombea, nyuma ya pazia analake jambo. Hii imenifanya nikumbuke lile soga la wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiongezea masurufu kwa madai maisha yamepanda. Kituko kilikuwa ni pale waziri mmoja alipoongeza nauli ya kivuko wabunge hao hao walikuja juu kama moto wa kifuu, tena kwa maneno ya kejeli ama kweli "Nyani haioni Kundule"

Huhitaji kuambiwa, "Ukiona chama au mwanasiasa anapuuzia kero za wapiga kura wake ujue HUYO/HAO hawa hitaji kura hizo kuingia madarakani, WANAZO MBINU ZINGINE ZA KUJICHAGUA AU KUCHAGULIWA, na huo ndio moshi unaofuka."

No comments:

Post a Comment