Friday, January 20, 2012

Tuache siasa Daktari Mmoja akigoma ujue kuna wagonjwa zaidi ya 20,000 hatarini: Madaktari na Walimu lazima wasikilizwe!!

Kwa muda mrefu Madaktari na walimu wamejikuta wakivaana na Serikali kwa kile wanachoamini UJIRA mdogo usioendana na uzito wa taaluma yao na hali duni ya maisha. Hili limepelekea kuzuka kwa migogoro ya mara kwa mara, na hatimaye MIGOMO ambayo huathiri walalahoi. Lakini swali muhimu ambalo kila Mtanzania anapaswa kujiuliza ni kwamba, "Serikali inatambua Athari za kuweka Umwamba wa Kisiasa katika hali kama hizi?"

Hivi Karibuni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya aliingia mitini baada ya kuombwa na chama cha madaktari kuhudhuria mkutano ili kujadili changamoto wanazozipata na msimamo wa serikali katika kutoa ufumbuzi. Mama huyu bila aibu aliamua "kuuchuna" pamoja na kutoa ahadi ya kuhudhuria baada ya saa moja. Labda tuendelee kujiuliza, anatoa wapi jeuri ya kugomea wito unaoendana na kazi aliyopewa?

Tuanze hapa: 1. Wanatibiwa wapi? Tumezoea kusikia vigogo wengi ndani ya serikali wakipeperuka na kwenda kutibiwa majuu, Rais anashikwa na kikozi anakimbilia Ujerumani kucheck, Katibu Mkuu nae Ufaransa, Mkurugenzi atasogezwa India basi ilimradi waende kutibiwa nje. Na sasa hata wabunge wameingizwa kwenye "system hiyo" kwanini washtushwe na madai ya Madaktari wa Maskini ambao hawaguswi na migomo yao? Takwimu zinaonyesha kuwa katika wagonjwa 10,000 kuna Daktari 0.5... kifupi daktari mmoja anatibia wagonjwa 20,000 hadi 45,000 hii haitoshi kusikiliza madai yao? Lakini kwa vile wao hawapo kwenye orodha hii pengine ndo maana hawaoni sababu ya kuogopa migomo ya wataalamu hawa. Kwa taarifa yako tu, Ikitokea daktari mmoja akagoma basi kuna wagonjwa 20,000 wataseka kama si kupoteza uhai.

Pili: Walimu nao wako kwenye mstari huu huu japo kwa sasa wamepumua, lakini tunakumbana na hali ile ile, watoto wa vigogo hatuwaoni kwenye shule zetu za kata japo tunaishi nao pale magogoni, nilisikia tetesi mtoto mmoja wa mzito wa nchi anasoma pale Upanga shule moja ya kiislam, cha kushangaza nasikia shule ile haifundishi somo la historia. Sasa huyu bila shaka atakuja kuingia kwenye siasa na kumrithi mzee wake. Sipati picha mkuu wa nchi au waziri asiyejua historia ya nchi yake, loo..pishilia mbali, itakuwa balaa mara dufu. Hii ndo sababu kubwa inaowapa jeuri viongozi wetu kupuuzia masuala ya msingi ya wataalamu wetu. Haingii akilini Taaluma kama ya udaktari, mtu anatumia nusu ya maisha yake kusoma na kusoma afu anakuja kulipwa mshahara ambao hata Kondakta wa daladala anamshinda. Ndio sijatia chumvi, Kondakta kwa siku anajilipa kati ya 15,000 hadi 20,000 kwa hesababu za haraka kwa mwezi anakamata kama laki sita "untaxed cash". 

Ukiniuliza mimi, ntakwambia hivi, "Wanajua umuhimu wenu ila wamechagua kuwapuuzia kwa kuwa wao wataenda US ambako madaktari wa kumwaga, nyie mtaendelea kutuulia ndugu zetu kwa kuwa mko wachache na mnatumia muda mwingi kusaka tonge." Hatuwalaumu ila tunajua cha kufanya 2015.

"In the U.S., if you fell ill and you're taken to hospital, you are going to meet a doctor. In my country, that's a luxury. A lot of people have gone to their graves without meeting a doctor." Dr. David Mwakyusa, former Minister of Health, Tanzania

No comments:

Post a Comment