Sunday, January 22, 2012

ARVs tumaini jipya linalokwazwa na ubishi wa kisiasa!!

MASWALI ya kisayansi yameibuka kuhoji utaratibu unaotumiwa na wahudumu wa afya katika kuwaanzisha Dozi za ARV watu wanaoishi na VVU sehemu mbalimbali duniani. Kwa mujibu wa shirika la Afya la Umoja wa Maitafa, watu wanaoishi na Virus vya Ukimwi wanashauriwa kuanza kutumia Dawa za kurefusha Maisha wanapofikisha CD4 chini ya 350 hadi 250. Hoja hii imekuja baada ya kugundulika kuwa Dawa hizo pamoja na kupunguza nguvu za virus vya HIV pia zinaweza kusaidia kupunguza maambukizi kwa asilimia 96 baina ya wahusika.

Kawaida mwili wa binadamu mwenye afya huwa na CD4 kati ya 500 hadi 1500. Virus vya Ukimwi vinapoingia mwilini hushambulia CD4 na T-cells ambazo ni muhimu katika utendaji kazi wa mfumo wa ulinzi ndani ya mwili. Matokeo ya uvamizi huu ni kushindwa kwa mwili kujitengenezea kinga na hivyo kuvamiwa kirahisi na magonjwa mengine. Matokeo mbalimbali ya kitafiti yameanza kuonyesha kuwa dawa za kurefusha maisha si tu zinasaidia kuongeza CD4 lakini pia zinaweza kutumika kama kinga baina ya mtu mwenye VVU na asiye na VVU endapo atatumia dozi ipasavyo.

Muongozo wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) umependekeza muda muafaka wa kuwaanzishia dozi za ARV watu wanaoishi na VVU ni pale wanapofikisha CD4 katika ya 350 na 250, hata hivyo hakuna utafiti wowote uliofanywa kuthibitisha madhara au faida ya kuanzishia dozi hiyo mapema jambo linaloibua shaka na utaratibu huo. Zipo hoja kadhaa zinazopelekea kuibuka kwa mtazamo mpya wa suala hili;
    1. Matokeo ya utafiti mpya unaothibitisha kuwa Dawa za ARV zinaweza kutumika kuzuia maambukizi ya VVU. Wahusika katika hoja hii wanatumia udhoefu wa muda mrefu wa ARV unaotokana na matumizi yake katika kuzuia maambukizi baina ya Mama na Mtoto (PMTCT) na hata miongoni mwa Wahudumu wa Afya pale wanapopata maambukizi wakati wanapotoa huduma kwa wagonjwa au waathirika wa VVU/Ukimwi (PEP). Hii inatosha kuthibitisha ukweli wa matokeo ya awali ya uwezekano wa ARV kutumika kuzuia maambukizi kwa makundi mengine ya jamii. 

   2. Hoja nyingine ni ile inayohusisha na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa ukimwi katika nchi zinazotumia utaratibu au muungozo wa Shirika la Afya, WHO. Kwa mfano mwaka 2009, Tanzania ilipoteza watu 86,000 kwa ugonjwa wa ukimwi na mwaka huo huo kulitokea maambukizi mapya 100,000. Hii pia inathibitisha kushindwa kwa nia ya awali ya kupunguza vifo kwa walioathirika na Ugonjwa huo na hivyo uhitaji wa kutafuta njia mbadala.

    3. Hoja ya tatu ni ile ya muda muafaka wa kuanza dozi. Mara nyingi watu wenye CD4 350 na 250 huwa katika hatua ya mwisho ya kuugua Ukimwi na huchukua muda mrefu kurejea katika afya yao ya kawaida baada ya kuanza dozi. Kutokana na changamoto zingine za kijamii na kiuchumi, wengi hushindwa kuendana na masharti ya dawa na wakati mwingine huwa katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi ikiwemo Kifua Kikuu, Kansa, matatizo ya Ini na kadhalika, ambapo humfikisha mgonjwa katika hali mbaya na hatimaye kifo.

    4. Mwisho, ni suala la nchi zilizoendelea kama Marekani na Ulaya kukataa kufuata muongozo wa Shirika la Afya. Kwa mfano Marekani humuanzishia mgonjwa dozi mara anapogundulika na VVU au anapofikisha CD4 500. Hizi ni taarifa mbaya kwa shirika la afya duniani, SWALI gumu ambalo nimekosa  jibu ni Sababu zipi zimewafanya waje na utaratibu huu ambao haukufanyiwa utafiti kikamilifu. HAKUNA MAJIBU YA KISAYANSI.

Kutokana na Hoja hizi wadau mbalimbali wa afya wameanza kupigia kampeni kuondolewa kwa muongozo wa WHO na kuangalia uwezekano wa kutafiti njia mbadala ikiwemo kutumia dawa za ARV katika mipango ya kuzuia maambukizi badala ya kutumika kama tiba peke yake.

Maneno ya Hisia tu, “Some epidemiological evidence suggests that HIV-infected patients remain healthier when they begin treatment at higher CD4 counts. However, there are also concerns about the health complications and side effects associated with lifelong antiretroviral use and the possibility that the virus may become resistant to medication,” Anthony S. Fauci, M.D. Mkurugenzi, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya kuambukiza, Marekani 

Tembelea www.niaid.nih.gov/topics/HIVAIDS kujua tafiti zinazohusu HIV/AIDS.

No comments:

Post a Comment